Nawezaje Kutambua kwamba Biblia ndilo Neno la kweli la Mungu?

Nawezaje Kutambua kwamba Biblia ndilo Neno la kweli la Mungu?

Mungu Mwumbaji wa vitu vyote hujifunua kwetu kwa namna tofauti tofauti. Viumbe vya asili kwa namna ya ajabu hushuhudia juu ya uwepo wake, uweza wake na tabia yake. Lakini Mungu hakuishia kujifunua kwetu kupitia viumbe vya asili pekee, amejifunua kwetu kupitia Maandiko Matakatifu yalioandikwa nyakati nyingi zilizopita yakielezea juu ya Mungu Mwumbaji wa vitu vyote.

Wengi twafahamu kwamba Mungu anayo Maandiko yake Matakatifu, lakini swali la muhimu linabaki, Ni maandiko yapi hayo? Kwani katika kipindi tunachoishi vimekuwepo vitabu vingi sana vinavyodaiwa kuwa vya Mungu, hivyo wengi hubaki njia panda wakijiuliza kwamba Kitabu kipi ndicho cha Mungu kweli? maana vitabu hivyo hutofautiana na kuhitilafiana sana kwa namna vinavyo muwasilisha Mungu.

Ipo habari njema kwa wote wanaotafuta kutambua ukweli kuhusu Neno la Kweli la Mungu ni lipi, nayo ni hii...

Mungu wetu ni mwenye upendo Mkuu, hivyo anahitaji kila mmoja aweze kutambua ukweli kuhusu Maandiko yake matakatifu kwani Maandiko yake hufunua namna Yeye alivyo, na hivyo Mungu Mwenyewe amelithibitisha Neno lake kwa ushahidi utoao uthibitisho wa ajabu na kushangaza sana, uthibitisho usio kuwa na uwezakano wa kawaida wa kibinadamu... Na Neno lake Hilo ni huitwa Biblia, vipo maelfu ya vithibitisho vinavyosimama kupiga kelele kwa wote kwamba Biblia ndilo Neno la Kweli la Mungu, na vithibitisho hivyo havina uwezekano wa kibinadamu kabisa, maana yake, ni vithibitisho vya hakika visivyoweza kutungwa na wanadamu. Leo ukijaribu kuangalia ushahidi unaotolewa katika kujaribu kuthibitisha madai ya vitabu vingi vinavyodaiwa kuwa vya Mungu utagundua kwamba vithibitisho hivyo ni vyenye uwezekano wa kawaida kibinadamu. Lakini ukirejea kwa Neno la Mungu utashangazwa kwa maajabu ya Vitibisho vyake.

Je Biblia hujishuhudia yenyewe kuwa ndilo Neno la Mungu?

Kabla ya kuangalia vithibitisho vinavyothibitisha kwamba Biblia ndilo Neno la Mungu ni muhimu kutambua kwamba, Biblia yenyewe hujishuhudia kwamba ndilo Neno la Mungu, maana ingekuwa haina maana kusema Biblia ni Neno la Mungu pasipo yenyewe kutuambia jambo hilo. Biblia husema Maandiko yake yana 'pumzi ya Mungu'(2 Timotheo 3:16) na 'iliandikwa kwa uongozi wa Roho wa Mungu' (2 Petro 1:21). Hivyo basi twaweza kusema bila hofu kuwa Biblia ndilo Neno la Mungu na pia mara kwa mara waandishi wa Biblia walitumia maneno kama 'Mungu asema', 'Bwana asema' n.k. kuonesha kwamba yalikuwa ni maneno ya Mungu waliyoyaongea ama kuyaandika.

Je ni ushahidi upi unaothibitisha ukweli kwamba Biblia ndilo Neno la Mungu?

Upo ushahidi mwingi unaothibitisha kuwa Biblia ni ya kweli na ndilo Neno la kweli la Mungu. Hapa chini ni baadhi ya ushahidi huo.

1. Unabii wa Biblia (Utabiri wa Mambo yajayo)

Ndani ya Biblia zimo tabiri nyingi za mambo ya mbele zilioandikwa miaka mingi kabla haijatokea. Unabii wa Biblia si kama tabiri za wanajimu leo, tabiri zinazopatikana katika kurasa za Biblia ni hakika kwani zote kwa namna ya ajabu hutimia sawa sawa na zilivyotabiriwa.

Biblia ina maelfu ya unabii katika agano jipya na agano la kale ambazo kadri tunapochunguza historia ya Dunia tunaona utimilifu kama zilivyoandikwa wake kwa namna ya pekee sana.

Unabii mwingi unapatikana katika Biblia kuhusu falme mbalimbali ambazo zingekuja kuinuka katika dunia, kama vile Uamedi na Uajemi, Uyunani, Rumi n.k. Pia Upo Unabii mwingi kuhusu watu mbalimbali, watu ambao walielezwa kuwepo kwao na mambo watakayoyafanya miaka mingi kabla hawajazaliwa, mfano Koreshi na Mwokozi wa Wanadamu, Yesu Kristo.

Unabii wa Biblia huthibitisha kwa namna ya kushangaza sana ukweli kwamba Biblia ndilo Neno la Kweli la Mungu.

2. Umoja wa Biblia

Biblia si kitabu kimoja bali ni mkusanyiko wa vitabu sitini na sita,vilivyoandikwa na waandishi takribani 40 waliokuwa na shughuli mbalimbali za kimaisha wengine wakiwa wavuvi, wafalme, wachunga kondoo, matabibu n.k. katika kipindi cha zaidi ya miaka 1500 ndani mabara matatu (Ulaya, Afrika na Asia) na ajabu zaidi wengi wa waandishi hao hawakuwahi kuonana lakini bado ukiisoma vitabu vyake sitini na sita Biblia ina umoja na mwafaka wa kushangaza katika ujumbe wake. Umoja huu huthibitisha kwamba Mungu mwenyewe ndiye aliyewaongoza waandishi wote kuandika kile alichokusudia.

3. Historia

Historia kwa namna ya ajabu hutoa ushahidi wa usahihi Biblia kupitia kwa uvumbuzi wa elimu mambo ya kale (Akiolojia) imethibitisha kwa namna ya kuvutia sana kwamba Biblia ni kweli na sahihi. Wanahistoria wamevigundua vibao vya udongo wa mfinyanzi pamoja na majengo ya kumbukumbu ya mawe ambayo yameonyesha majina, mahali, na matukio yaliyojulikana kuhusu siku za nyuma kutokana na Biblia tu. Mfano miji mbalimbali iliyotajwa katika Biblia imekuja kuthibitika kupitia mavumbuzi ya elimu ya mambo ya kale kwamba ilikuwepo na matukio yaliyoelezewa katika Biblia yalitokea kweli. Miji kama vile Sodoma na Gomora, Babeli, Tiro n.k.

Lakini pia kupitia vyanzo mbalimbali vingine vya kihistoria Biblia imeendelea kuthibitishwa kuwa ni kweli kwani hata watu mbalimbali waliotajwa katika Biblia huonekana katika nakala nyingine za Historia wakiwa wamefanya matukio yale yale yalioelezwa katika Biblia. Mfano Mfalme Daudi, Nebukadreza na hata Yesu Kristo.

4. Sayansi

Hata katika Elimu ya Sayansi upo ushahidi mwingi sana unaotuthibishia kuwa Biblia ndilo neno la kweli la Mungu. Mfano ni kauli za kushangaza za Biblia kuhusu sayansi kama vile inayopatikana katika Ayubu 26:7, Biblia inasema

Yeye hutandaza kaskazi juu ya nafasi isiyo na kitu, Na kuutundika ulimwengu pasipo kitu."

Ayubu aliishi maelfu ya miaka iliyopita, zamani ambapo hakukuwa na mtu aliyefahamu kuwa dunia huelea yenyewe angani bali watu walidhani kuwa dunia hushikiliwa na kitu flani. Ni katika karne za karibuni ndipo imethibitika kwa sayansi kuwa dunia huelea angani.

Pia katika Isaya 40:22 hueleza kwamba dunia ni duara. Katika mwaka 1492 Christopher Columbus alikuwa akijaribu kutafuta mahali palipokuwa na ukingo wa dunia. Watu kipindi chake waliamini kuwa dunia ipo flati. Kama angetazama Biblia angeweza kufahamu Dunia haipo flati hata kabla sayansi haithibitisha

5. Kuhifadhiwa kwa Biblia

Mamillioni kwa karne nyingi wamekuwa wakijaribu kuiangamiza Biblia. Mfano Katika kipindi kijulikanacho kama 'zama za giza' Maadui wengi wa Biblia walijaribu kuipoteza Biblia isiwepo mikononi mwa watu, na ajabu zaidi watu walioaminiwa, wenye cheo katika dini ya Ukristo wa kipindi hicho ndio waliokuwa mstari wa mbele kutaka kuikomesha Biblia. Watu wa kawaida waliwekwa gerezani na wakati mwingine kuuawa kwa kukutwa na Biblia au kufundisha wengine mafundisho yake. Historia inatuambia kwamba wanamatengenezo walikiuka sheria hizo kwa kujisomea Biblia wenyewe na kuwafundisha wengine.

Hata hivyo, licha ya majaribio yote ya watu waliojaribu kuitokomeza Biblia, Biblia bado inaendelea kuwa kitabu kiuzwacho zaidi duniani kila mwaka.

Isaya 40:8 inasema

Majani yakauka, ua lanyauka; Bali Neno la Mungu wetu litasimama milele."

Hakika Neno la Mungu litasimama milele, mwanadamu haweza kuliangamiza wala kulinyamazisha, litaendelea kuwepo hadi mwisho wa wakati.

6. Nguvu ya kubadilisha maisha

Neno la Mungu kwa maelfu ya miaka sasa limeendelea kubadili maisha ya mamillioni ya watu.Ipo nguvu ya pekee katika Neno la Mungu ambayo huwabadilisha wote wasomao, kuyaamini na kuyashika maneno yake. Zipo shuhuda nyingi za watu waliokuwa majambazi, wahanga wa madawa ya kulevya, washirikina na kila aina ya mienendo mibaya wabadilika na kuwa wema kutokana na Neno la Mungu, Biblia. Biblia inasema katika 1 Petro 1:23

Kwa kuwa mmezaliwa mara ya pili; si kwa mbegu iharibikayo, bali kwa ile isiyoharibika; kwa Neno la Mungu lenye uzima, lidumulo hata milele."

Ni kwa kupitia Neno la Mungu pekee mtu aweza kupata badiliko la kweli, wanadamu tunamwelekeo wa asili wa kufanya maovu, lakini kupitia nguvu ya Neno la Mungu, hutusaidia 'kuzaliwa mara ya pili', kuwa na nia mpya (Warumi 12:1,2), kuwa kiumbe kipya (2 Wakorintho 5:17) na kushinda dhambi katika maisha yetu.

Hitimisho

Je Biblia ndilo Neno la Kweli la Mungu? Jibu ni Ndiyo, Mungu anatualika kila mmoja wetu akisema "Onjeni mwone ya kuwa Bwana yu mwema" Zaburi 34:8. Haiwezi kujua radha halisi ya kitu alichoonja mtu mwingine, ni lazima kujionjea mwenyewe. Mungu anakualika nawe rafiki mpendwa leo jionjee mwenyewe. Namna ya kuonja ni kwa kulisoma Neno lake, jionjee mwenyewe leo kwa kujifunza Biblia yako mwenyewe si kwa kutegemea namna wengine wasemavyo.

Mpya kutoka kwetu