Mkate wa Kila Siku

Mkate wa Kila Siku

“Imeandikwa, Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu.” Mathayo 4:4

Ni maneno aliyoyasema Mwokozi wetu Yesu Kristo alipokuwa hapa duniani pale mjaribu alipomjia.

Biblia ni Neno la Mungu, baadhi wamekuwa wakikichukulia kama kitabu chenye maelekezo na masharti fulani yakufuata tu pasipo kuwa na uhalisia katika maisha ya kila siku, na wengine wamekuwa wakiiona Biblia kama kitabu cha kuthibitishia mafundisho ya kidini kwa nadharia tu pasipo kuwa na mguso katika maisha ya kila siku. Lakini si kweli, Ukweli ni kwamba Biblia ni zaidi ya namna ambavyo wengi leo tunaichukulia, kwani “neno la Mungu li hai” (Waebrania 4:12).

Leo nataka tujifunze mambo matatu ya kuzingatia ambayo yaweza kutusaidia katika usomaji wetu wa Biblia, kutuweza kuona namna ambavyo Neno la Mungu linagusa maisha yetu ya kila siku. Nayo ni haya...

Kwanza kabisa usomapo fungu au kifungu fulani cha Biblia tambua kwamba kuna pambano linaloendelea, baina ya uovu na wema katika nyakati husika za tukio ulilosoma ndani ya Biblia na hata leo hii. Jihoji maswali mengi kama vile, kifungu au fungu hili linaniambia nini kuhusu pambano kuu, jiulize ni jambo gani ambalo mwandishi alikusudia kuandika. Kwa mfano usomapo vitabu vya nyaraka jiulize nini kilimpelekea mwandishi aandike waraka huu, alikuwa na lengo gani ukilinganisha na fungu au kifungu chako, kulikuwa na jambo gani liliyopemlekea kuandika. Ili kuelewa haswa lengo la mwandishi ni vyema kusoma mafungu kadhaa kabla na baada ya fungu au kifungu cha aya unachokisoma.

Pili usomapo fungu au kifungu chako jiulize unapata ujumbe gani kumhusu Mungu, yaani kuhusu upendo wake, tafuta kufahamu kwa undani zaidi kuhusu upendo wa Mungu, maana upendo wa Mungu ndio ujumbe Mkuu uliosheheni kila kurasa na kila kifungu cha Biblia, upendo wa Mungu kama unavyoonekana pale Msalabani ndiyo ujumbe kuu wa Biblia.

Mwisho, usomapo fungu au kifungu cha Biblia ona namna ambavyo waweza kutumia ulichosoma katika maisha yako, kutokana mambo uliyoyagundua kuhusu pambano kuu na upendo wa Mungu katika fungu hilo, fikiria ni sehemu gani katika maisha yako zinazohitaji marekebisho, mwombe Mungu kupitia Roho wake akuoneshe mambo ya kufanyia marekebisho katika maisha yako ya kila siku.

Hayo ndiyo mambo matatu ambayo yaweza kukusaidia katika usomaji wako wa neno la Mungu, kuona namna ambavyo Neno la Mungu linagusa maisha yako ya kila siku. Ni mapenzi ya Mungu kwamba kila siku tuishi kwa ‘neno litokalo kwake’, kila siku tukibadilishwa kufanana naye.

Mpya kutoka kwetu