Vyote Kwa Ajili Yako

Vyote Kwa Ajili Yako

Katika Sura ya Kwanza na ya pili ya kitabu cha Mwanzo, Biblia hueleza namna ambavyo Mungu aliiumba dunia yetu. Dunia ilipotoka mikononi mwa Mwumbaji ilikuwa yenye uzuri usio na kifani, hakukuwa na hali yoyote ya uharibifu. Katika kilele cha uumbaji wake Mungu, Biblia hutueleza kwamba Mungu alimwumba mwanadamu katika siku ya sita na kumweka katika bustani.

“Bwana Mungu akapanda bustani upande wa mashariki wa Edeni, akamweka ndani yake huyo mtu aliyemfanya.” Mwanzo 2:8

Bustanini, ndiyo makazi ambayo Mungu alipanga wanadamu waishi humo siku zote za maisha yao. Hebu jaribu kufikiria juu ya uzuri wa bustani nzuri uzijuazo leo, bustani za miti ya matunda na maua, namna hewa ilivyo safi, harufu nzuri ya maua, milio mizuri ya ndege na mengine mengi ya kuvutia ndani bustani. Sasa hebu fikiri juu ya uzuri wa ile bustani ya kwanza iliyoumbwa na Yeye mwenye hekima, uweza na maarifa yote, kweli uzuri wake ulikuwa hauna kifani, Lakini, Kumbuka yote Mungu aliyafanya kwa ajili ya Mwanadamu!

Ingawa dunia imeanguka katika hali mbaya kwa ajili ya dhambi lakini yote yaliyomo si huzuni na na mashaka tupu. Viumbe vya asili vimekuwa wajumbe wa Mungu kutuletea maneno ya kututia faraja na kutuliza roho zetu. Kila mti wa miiba una maua yake; yaani katika kila shida twaweza kupata baraka za Mungu. “Mungu ni upendo” imeandikwa kila mahali. Ndege waimbao vizuri, kila aina ya maua na miti, yote hutushuhudia juu ya upendo na uangalifu wa Mungu, jinsi atakavyo kuwafurahisha watoto wake.

Shetani amepofusha macho ya wanadamu ili wamwogope Mungu. Yeye hufanya kazi ya kuwapoteza wanadamu ili wamdhanie Mungu kama mkali na asiye na huruma kabisa, kama jaji aliye na roho ngumu asiyeweza kumwachia Mtu. Huwatilia wanadamu fikra kwamba Mungu huwachungachunga ili apate kujua makosa yao na kisha kuleta hukumu zake juu yao.

Bwana Yesu alikuja hapa duniani na kuishi kati ya wanadamu kwa kusudi la kuwaondolea wanadamu fikra zao mbaya kumhusu Mungu, kuwaonesha halisi namna Mungu alivyo, Yesu alisema

“Aliyeniona mimi amemwona Baba” Yohana 14:9

kwa maisha aliyoishi hapa Duniani, Bwana Yesu alionesha kuwa Mungu ni upendo katika matendo yake, kwa namna alivyowajali na kuwapenda watu wote, namna alivyokuwa mwepesi kuwaondolea wanadamu maumivu, namna alivyowaweka huru walioteswa. Na zaidi kabisa kwa kifo chake msalabani Bwana Yesu alituonesha upendo mkuu wa Mungu wetu.

“Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake.” Yohana 15:13

Rafiki Mungu wetu amefanya mambo yote kwa ajili yako, amekupatia uzuri wa viumbe vya asili ili upate furaha kwa namna vinavyomfunua yeye, na zaidi akamtoa mwanawe afe ili upate kuishi, yote ni kwa ajili yako. Mpokee Mungu leo kwani anakupenda sana na anataka awe Rafiki yako leo.

Mpya kutoka kwetu