Aliye wa Kuaminika Kuliko Wote

Aliye wa Kuaminika Kuliko Wote

Maandiko matakatifu pamoja na viumbe vya asili hushuhudia juu ya uweza na nguvu za Mungu wetu. Katika viumbe vya asili tunapotazama vitu vya ajabu alivyoviumba Mungu ni dhahiri kuwa hakuna jambo gumu kwake.

Hebu tazama angani wakati wa usiku, ona ambavyo anga limejawa na mabillioni ya nyota, nyingi mno ambazo hata kwa vifaa vya namna gani akili za mwanadamu haziwezi kutambua idadi yake, lakini ajabu Mungu wetu sio tu kwamba anafahamu idadi yake, bali pia huziita zote, moja moja, kwa majina (Zaburi 147:4).

Biblia hutuambia kuwa,

“Kwa Mungu yote yanawezekana” (Mathayo 19:26)

wanadamu kwa akili zetu hatuwezi kutafakari juu ya uweza wa Mungu na kuelewa kikamilifu, Mawazo yake na njia zake ni kuu mno (Isaya 55:8-9).

Pamoja na kuwa na Uweza mkuu wa kutoshindwa na lolote pia Mungu wetu anafahamu mambo yote ikiwemo yaliyokwisha kupita, mambo yaliyopo na mambo yatakayo kuja, yeye huiandika historia kabla haijatokea, yaani, Yeye hujua mwisho wa jambo kabla mwanzo wake haujafika (Isaya 46:10).

Ni jambo zuri namna gani kwamba Mungu wetu ni mwenye nguvu na uweza wote, hekima na maarifa yake havina kikomo, hivyo mpendwa twaweza kuwa na hakika kabisa kumkabidhi maisha yetu, kwani hakuna jambo lilsilowekezekana kwake. Yeye ndiye aliye wa kuaminika kuliko wote, hatotuangusha kamwe. Yeye hutujali na yupo nasi katika hali zote.

Siri ya ukweli huu mkuu kwamba Mungu wetu ndiye wa kuaminika kuliko wote inapatikana katika kifungu kimoja cha maandiko kisemacho “Mungu ni Upendo” 1 Yohana 4:8. Licha ya kuwa nguvu na uweza usio na ukomo, hatushinikizi kuwa marafiki zake, badala yake anagonga taratibu katika mioyo yetu, akiomba tumfungulie.

Mungu wetu ni wa ajabu sana rafiki, upendo wake hauna kifani. Ni nafasi ya pekee namna gani hii rafiki, mfungulie moyo leo Mungu kwani anakupenda sana.

Mpya kutoka kwetu