Macho Yote Kwako

Macho Yote Kwako

Sayari yetu, Dunia, ni sayari ndogo sana katika ukubwa wa anga la Ulimwengu wote aliouumba Mungu. Watafiti wa mambo ya anga wanapoitazama Dunia kwa nje kwa kutumia vyombo vyao vya anga hushangazwa na udogo wa Dunia unaodhihirika pale inapolinganishwa na ukubwa wa anga.

Katika mwaka 1990 chombo cha anga cha Marekani kilichoitwa Voyager kilifanikiwa kupiga picha za anga kikiwa nje ya sayari yetu umbali mrefu sana. Moja kati ya picha hizo iliyopewa jina "pale blue dot", yaani doti la rangi ya bluu mpauko, ilionesha kwa halisi namna ambavyo Dunia yetu ilivyo ndogo, kulingana na picha ile namna Dunia yetu ilivyoonekana katika ukubwa anga, ni kama doti dogo katika karatasi kubwa nyeupe, yaani sawa na alama ya nukta (‘.’) katika karatasi kubwa nyeupe.

Ni kweli kwamba Dunia yetu ni ndogo, ndogo sana, katika ukubwa wa anga la ulimwengu, lakini cha kushangaza ni kwamba dunia yetu na sisi wakazi wake tunathamani kubwa! kubwa sana katika macho ya Muumbaji wetu. Baada ya kutafakari juu ya ukubwa wa anga la ulimwengu, Mfalme Daudi, aliomba maneno haya,

"Mtu ni kitu gani hata umkumbuke. Na binadamu hata umwangalie" Zaburi 8:3-4.

Jibu rahisi linatolewa na Biblia ni kwamba binadamu anathamani kubwa sana kwa Mungu, rahisi na hakika, kwa sababu Mungu anatupenda, tunaambiwa na Manabii wa kale kwamba Mungu anatufahamu kila mmoja wetu kwa jina kabla hata hatujazaliwa (Yeremiah 1:5, Zaburi 139:16), humjali kila mmoja na ameweka uangalizi wake wote kwa kila mwanadamu kana kwamba yupo peke yake anaye mjali dunia nzima, hujihusisha kwa karibu na kila mmoja wetu, kwa karibu zaidi ya vile Mama anavyomjali mwanawe ampendaye. Kila asubuhi unapoamka, Biblia husema macho yake yapo juu yako, hufurahi kukuona daima ukiwa mwenye furaha, macho yako yanapotoka machozi huona na kuusikia uchungu wako, maumivu na mateso yanayosababishwa na maamuzi mabaya ya wanadamu huchoma moyo wa Mungu.

Rafiki yangu, ni furaha iliyoje kutambua kwamba yupo anayetujali na kutulinda katika hali zote, macho yake daima yako juu yetu, yeye hutuwazia mema siku zote, hebu rafiki jikabidhi kwake Mungu leo kwani anakupenda sana.

Mpya kutoka kwetu