Aliye Karibu Kuliko Wote

Aliye Karibu Kuliko Wote

Mauvimu, shida na matatizo ni humuhangaisha kila mkazi wa sayari yetu, japo kwa namna na hali tofauti tofauti, kila mmoja wetu hujikuta mara kwa mara katika matatizo. Ni kawaida kwa wanadamu kijiuliza swali la muhimu, kwamba "Mungu yuko wapi katika haya ninayoyapitia?" au "Mungu ananijali kweli?" na maswali mengine mengi ya namna hii.

Mbaya zaidi ni kwamba dunia yetu imejawa na mitazamo mibaya na taswira mbaya kumhusu Mungu. Katika historia yote ya wanadamu tangu dhambi iingie duniani hadi sasa wanadamu wengi wamebeba akilini mwao mitazamo mibaya kuhusu Mungu anavyohusiana nasi.

Wanafalsafa maarufu wa Kigiriki, Plato na Aristotle katika falsafa zao walipendekeza kwamba Mungu yupo mbali kabisa na hahusiani na chochote kinachoendelea katika ulimwengu aliouumba, kiasi kwamba walisema 'Mungu hana hisia' zozote juu ya wengine. Wakitetea hoja zao walisema kwamba kama 'Mungu ni mkamilifu, basi hawezi kupata badiliko lolote ndani yake [yaani badiliko la hisia]'.

Sio katika falsafa za Kigiriki pekee tangu awali hii ndiyo imekuwa kampeni ya shetani, kwamba Mungu hajihusishi nasi, kwa lugha nyingine ni sawa na kusema kuwa Mungu hana upendo, hawajali wengine na yupo kwa ajili ya maslahi yake pekee.

Mitazamo hii kumhusu Mungu imepenya hata katika imani na dini za wengi leo. Wengi leo hata wanaodai kuwa wafuasi wa dini wana mitazamo hii mibaya kumhusu Mungu. Hivyo wengi hufikiri kwamba katika maumivu na shida zao hawana msaada kwani hata aliyewaumba hawajali.

Jambo la kushukuru ni kwamba mitazamo hii juu ya Mungu si ya kweli, na wala si sahihi. Biblia hutueleza kwamba Mungu hujihusisha na kujishughulisha sana na mambo yetu, yeye anatupenda, na kutuwazia mambo mema siku zote, hatuachi peke yetu kusumbuka na matatizo yetu wenyewe.

Mfano rahisi, Nabii Isaya alipokuwa akizungumza juu ya wana wa Isreali namna walivyokuwa wakipitia mateso Nabii Isaya alisema,

"katika mateso yao yote, yeye aliteswa" Isaya 63:9

'Yeye aliteswa!' kinyume kabisa na mapendekezo ya ulimwengu huu, Mungu alikuwa karibu sana na wana wa Israeli kiasi kwamba katika kuteswa kwao ni sawa na kama Yeye alikuwa akiteswa. Na Mungu yupo pamoja nasi leo katika shida zetu kama ilivyokuwa kwa wana wa Israeli, anaona mahangaiko yetu. Yupo nasi kama ilivyokuwa kwa Shedrack, Meshack na Abednego waliotupwa katikati ya tanuru liwakalo moto, Mungu hakuwaacha, alikuwa pamoja nao katikati ya ule moto.

Huu ndio ukweli rafiki, Mungu wetu anatujali sana, hujihusisha sana na mambo yetu wakati wote, katika matatizo yatupatayo yeye yupo nasi atuoneshe namna ya kuenenda na kutupatia farijiko, tumaini na msaada wakati wote. Na kama ilivyokuwa kwa wale vijana wakiebrania waliomtumaini Mungu hata ndani ya tanuru la moto na moto haukuwadhuru, vivyo hivyo nawe rafiki ukimtuamini Mungu katika shida na matatizo unayopitia, atakuwa nawe na shida na matatizo yako yatakuwa si kitu katika uwepo wake Mungu.

Mpya kutoka kwetu