Ingawa Hatukustahili

Ingawa Hatukustahili

Biblia inaeleza kwamba hapo mwanzo mwanadamu alikuwa mkamilifu katika mwili wake, fikara ilikuwa safi, makusudi yake matakatifu na alikuwa katika hali ya umoja na Mungu. Lakini kwa uasi aliounzisha mwanadamu, uwezo wake ulibadilika, fikara na makusudi yake yakawa maovu, na kwa ajili ya uasi wake mwanadamu, dhambi iliathiri dunia na kuleta uharibifu mkubwa mpaka leo hii.

Katika kitabu cha Mwanzo sura ya 3, huelezea namna ambavyo dhambi iliingia duniani, wanadamu walimwasi Mungu kwa kula matunda ya mti ambao Bwana Mungu aliwaambia wasile, kwani kama wangekula wangekufa. Biblia inaeleza kuwa mwanamke "alitwaa matunda yake, akala akampa na mumewe naye akala" (Mwanzo 3:6).

Kwa kula matunda ya mti ule wanadamu walitenda dhambi na,

"Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti" Warumi 6:23.

Adhabu ya kifo iliwastahili wanadamu wa kwanza, kifo cha milele. Na kama ilivyokuwa kwa wanadamu wa kwanza, leo pia adhabu ya kifo cha milele inatukabili wote tutendao dhambi. Lakini mpendwa ipo habari njema,

"Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele." Yohana 3:16

Mungu wetu ametupatia neema kuu namna gani, kifo cha Mwanawe pale msalabani kimelipa adhabu yetu ya mauti ya milele na kupitia Yeye tunalo tumaini la Kuishi Milele.

Ni kwa neema ya Mungu tu rafiki yangu tunalotumaini la kuishi milele. Lakini pia licha ya tumaini la kuishi milele, hata leo katika dunia hii tunazungukwa na mibaraka mingi ya Mungu ambayo hutupatia kwa neema yake kuu tu, hatukustahili lolote, fikiri juu ya pumzi unayovuta, haukuilipia chochote wala huwezi kuilipia, neema ya Mungu inatuzunguka kila mahali, Biblia inasema Baba wa Mbinguni

"huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki" Mathayo 5:45

Rafiki mpendwa, hatukustahili, lakini ni kwa neema ya Mungu, mibaraka yake inatuzunguka, ni kwa neema yake tuliondoalewa adhabi ya mauti ya milele na sasa tunalotumaini la uzima wa milele. Mungu anatupenda sana rafiki, hebu tumshukuru kwa neema yake kuu.

Mpya kutoka kwetu