Uvumilivu Mkuu

Uvumilivu Mkuu

Je umeshawahi kujiuliza kwa nini Mungu asiisimamishe dunia yetu hii mara moja hata sasa hivi, jaribu kufikiria kwa muda mfupi, dunia yetu imejawa shida nyingi, mateso, ugaidi na kila aina ya matendo ya ukatili. Labda pengine si rahisi kuona uzito wa jambo hili pasipokuwa mhanga wa mambo hatarishi yanaoendelea katika dunia, lakini hebu katika kufikiri jiweke katika mazingira ya 'mtoto yule mdogo ambaye ni mhanga wa vita au matukio ya ugaidi, mtoto mwenye umri mdogo sana ambaye wazazi wake waliuawa kikatili mbele ya macho yake, na sasa mtoto huyo amekilaza kichwa chake chini kwa taabu kutokana na mwili wake kukosa nguvu kwa kutokupata chakula siku kadhaa. Ukiwa Katika hali kama hii na ukapewa nafasi au uwezo wa kuisimamisha dunia wakati huu, nina hakika ungefanya hivyo.

Lakini, jambo la kushangaza ni kwamba Yeye aliye na uwezo wa kufanya hivyo, kuisimamisha duniani hata kwa wakati huu, Yeye, Mungu hachagui kufanya hivyo. Kwa nini?

Kwanza tambua kwamba Mungu anaona mambo mengi zaidi ya tunavyoweza kuona, anaona uwezo katika watu ambao kimsingi kwa macho ya kibinadamu hatuwezi kuuona, na muhimu zaidi Mungu anawapenda watu kwa upendo mkuu ambao kama wanadamu hatuna upendo huo.

Mungu kuacha dunia yetu kuendelea katika hali iliyopo sasa, si kwa sababu hahisi kinachoendelea, au anapenda kuona hivi, hapana, Kimsingi Mungu ndiye pekee mwenye uwezo wa kuhisi kila kitu kinachoendelea mahali popote na upendo wake ni mkuu sana, upendo wa kujitoa nafsi yake kwa ajili ya wengine! Lakini swali linabaki kwa nini bado anaacha mambo yanaendelea kuwa hivi leo duniani. Biblia hutoa majibu, ikisema katika 2 Petro 3:9

"huvumilia kwenu, maana hapendi mtu ye yote apotee, bali wote wafikilie toba" 2 Petro 3:9

Hapa ndipo ulipo ukweli rafiki, moyo wa Mungu wawekwa wazi kwetu, kwamba hapendi mtu yeyote apotee, anahitaji wokovu kwa kila mwanaume, mwanamke na watoto Yesu aliowafia. Angeweza kuisimamisha duniani hata muda huu, lakini pengine kwa ajili yangu au yako anaona anaweza kutuokoa. Anaona shida tunazopitia kama matokeo ya maamuzi yetu wenyewe mabaya au ya watu wengine na siku zote anatusihi tumkabidhi maisha yetu na milima ya shida zetu itageuka kuwa tambarare, Yeye hatuachi peke yetu katika magumu yupo nasi siku zote.

Rafiki yangu, Mungu anahitaji uweze kupata wokovu, ni matamanio yake aweze kukuokoa ili siku moja muishi naye mahali pamoja (mbinguni), yeye Mungu amefanya yote ili wewe uweze kuokoka, inabaki kwako rafiki kukubali kupokea wokovu huu. Biblia yasema,

"sisi je! Tutapataje kupona, tusipojali wokovu mkuu namna hii?" Waebrania 2:3

Mpya kutoka kwetu