Nini Chanzo cha Haya Yote

Nini Chanzo cha Haya Yote

Ukweli mkuu wa Biblia ni kwamba,

"Mungu ni Upendo" 1 Yohana 4:8.

'Mungu ni Upendo', kauli yenye nguvu namna gani! Lakini katika Dunia tunayoishi leo kauli hii huamsha maswali mengi kutokana na uhalisia wa hali ya Dunia yetu. Sote twatambua kwamba hali si shwari Duniani, kuna shida, dhiki na mahangaiko ya kila namna, kweli hali si shwari! Na hivyo wengi hujiuliza, 'kama Mungu ni Upendo (ana upendo) kwa nini dunia yetu ipi hivi leo, kwa nini kuna maumivu kiasi hiki duniani?' swali hili humsumbua kila mkazi wa dunia hii kwa namna tofauti tofauti, haijalishi ni mfuasi wa dini au la kwa namna moja au nyingine watu wote husumbuliwa na swali hili.

Biblia ipo wazi kuhusiana na hali iliyopo hapa duniani, Mwokozi wetu Yesu alisema,

"Ulimwenguni mnayo dhiki; lakini jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu." Yohana 16:33

Lakini Biblia inatueleza kwamba Mungu alipoiumba dunia kila kitu kilikuwa chema,

"Mungu akaona kila kitu alichokifanya, na tazama, ni chema sana." Mwanzo 1:31.

Hali ya mwanzo ya dunia yetu ilipotoka mikononi mwa Mungu njema sana, dunia ilikuwa isiyo na shida wala mahangaiko yeyote.

Swali linabaki, nini kilitokea kilichosababisha ulimwengu wetu kuwa katika hali yake leo?

Biblia hueleza namna ambavyo Dunia yetu imefikia katika hali iliyopo sasa kwa mfumo wa kisa, na kisa hiki chaweza kufupishwa katika maneno machache aliyoyasema Yesu alipokuwa akifundisha, katika kufundisha kwake alitumia mfano mmoja akieleza kwamba kulikuwa na konde (shamba) ambalo mwenye shamba alipanda mbegu nzuri tu. Lakini ajabu magugu yakaoneka, ndipo wafanyakazi walipomwendea mwenye shamba (Yesu) wakimwuliza magugu yametoka wapi, mbona tulipanda mbegu nzuri tu!, jibu la mwenye shamba (Yesu) lilikuwa

"Adui ndiye aliyetenda hivi" Mathayo 13:28,

Jibu fupi tu lenye maneno manne tu, lakini maneno haya machache yanaeleza ukweli mkuu kuhusu namna ambavyo dunia yetu imefikia katika hali yake ya sasa.

Ni Adui, 'Adui ndiye aliyetenda hivi'. Adui huyu Biblia humwita Shetani, na jambo la kushangaza ni kwamba Mungu hakumwumba kama adui bali alikuwa rafiki aliyekuwa mwema, mzuri na mtakatifu hapo awali, na akiwa mwenye uhuru wa maamuzi, naye alichagua mwenyewe kuwa mwovu na kuanzisha uasi ambao matokeo yake ameleta maumivu, magonjwa na shida za kila namna, vyote ni kutokana na uasi wake wa sheria ya Mungu, sheria ya Upendo.

Hivi rafiki ndivyo ambavyo dunia yetu imefika hapa leo katika hali yake hii ya shida nyingi, lakini katika yote "Mungu ni Upendo" (1 Yohana 4:8), kwani anafanya kazi kutusaidia kuturejesha katika mpango wake wa awali, mpango wa dunia isiyokuwa na shida wala mahangaiko ya namna yeyote. Nawe pia rafiki anakualika katika mpango wake wa kurejesha dunia katika uzuri wake, hebu ungana naye kwa kumkabidhi maisha yako ayaongoze kukuwezesha kufikia mpango huu.

Mpya kutoka kwetu