Zawadi Nzuri Lakini Yenye Hatari

Zawadi Nzuri Lakini Yenye Hatari

Kila mwanadamu anapenda kuwa huru, huru kufanya maamuzi yake apendavyo, kwa kawaida hakuna anayependa kutawaliwa kwa mabavu na mtu mwingine. uhuru wa maamuzi ni kitu muhimu sana katika maisha.

Lakini, ipo hatari katika uhuru wa maamuzi pale mtu anapoamua kutumia uhuru wake vibaya. Mfano halisi kisa cha namna ambavyo dunia yetu imefikia katika hali mbaya iliyo nayo sasa, yote ni kutokana na kutumia vibaya uhuru.

Kisa cha namna ambavyo uharibifu uliingia Ulimwenguni hushangaza sana. Biblia hueleza kwamba chanzo ilikuwa ni kiumbe mmoja wa Mungu, Malaika aliyeitwa Lusifa, kiumbe ambaye tunaambiwa na Maandiko Matakatifu alikuwa mzuri, mwema na mkamilifu hapo mwanzo Mungu alipomuumba (Ezekiel 28:13-15), Mungu wetu katika kumuumba Lusifa hakumnyima kiumbe huyu zawadi nzuri na muhimu ya ‘uhuru wa maamuzi’, maana Biblia inatuambia kwamba "Mungu ni Upendo" 1 Yohana 4:8 na hivyo ni upendo pekee Mungu anaohitaji, ili upendo uwepo lazima pawepo na uhuru wa maamuzi, lazima mtu awe huru kuchagua, maana upendo haulazimishwi.

Hivyo basi Mungu alimuumba Lusifa pasipo kumnyima zawadi iliyomuwezesha kuwa kiumbe mwenye uwezo wa kupenda, yaani zawadi ya Uhuru wa maamuzi.

Biblia inaeleza kwamba Lusifa aliasi kutokana kutumia vibaya uhuru wake, alijiinua nafsini mwake (Ezekiel 28:17) na kutamani nafasi ya Mungu. Nabii Isaya anasema haya kuhusu Lusifa...

"Nawe ulisema moyoni mwako, Nitapanda mpaka mbinguni, nitakiinua kiti change juu kuliko nyota za Mungu...nitapaa kupita vimo vya mawingu, nitafanana naye Aliye juu." Isaya 14:13.

Kama matokeo ya kuwa na ubinafsi moyoni mwake, kutamani madaraka ya Mungu, Lusifa aliamua kuasi na kuanzisha vita mbinguni (Ufunuo 12:7), vita ambavyo matokeo yake yameathiri hata Dunia yetu.

Mungu angeweza kumuangamiza Lusifa mara moja tu baada ya uasi wake, lakini hakuchagua kufanya hivyo, "Mungu ni Upendo", kwa kumuangamiza Lusifa pale pale ingekuwa kinyume na kanuni yake kuu ya Upendo kwani hata viumbe wengine wangehusiana na Mungu kwa kumwogopa si kwa upendo tena. Mungu alitazama uasi wa Lusifa na kuona kwamba suluhisho pekee la kudumu na la hakika linapatikana Msalabani. Mungu kwa upendo wake alikuwa tayari kumtoa mwanawe kufa ili kurejesha kila kilichopotea kutokana na uasi wa Lusifa.

Rafiki, hata leo mchakato wa Mungu wa kuirejesha Dunia katika uzuri wake wa awali unaendelea, kila siku tunapofanya maamuzi tukitumia uhuru tuliopewa tunakuwa tunashirikiana ama na Mungu katika urejeshwaji wa Dunia au tunashirikiana na Lusifa katika kuelekea upotovuni. Hebu jiulize Leo ‘ni nani unayeshirikiana naye, ni Mungu au Lusifa’. Tumia vizuri uhuru wako leo, mkabidhi Yesu maisha yako akuongoze kufanya maamuzi sahihi siku zote.

Mpya kutoka kwetu