Pambano Kuu - Mwanzo wa Pambano

Pambano Kuu - Mwanzo wa Pambano

Yeyote mwenye ufahamu atagundua kwamba mambo hayapo sawa katika dunia yetu, ni kama kuna kitu kisichokuwa cha kawaida kinaendelea. Kila tunapogeuka tunaona magonjwa, maumivu na shida za kila namna, hakika mambo hayapo sawa.

Biblia hutupatia maelezo ya kutosha kutusaidia kuelewa chanzo na muelekeo wa hali ya dunia yetu. Katika kurasa zake Takatifu, Biblia hueleza kwamba ndani ya sayari yetu kuna vita inayoendelea, vita kati ya wema na uovu, kati ya ukweli na uongo. Vita hii wengi wameiita "PAMBANO KUU"

Jambo la kushangaza Biblia hueleza kwamba vita hii haikuanzia hapa dunia, ilianzia katika makao makuu ya ulimwengu, yaani, Mbinguni. Kutokana na uasi wa mmoja kati ya Malaika wa Mungu, aliyeitwa Lusifa, ambaye hapo mwanzo alipoumbwa na Mungu alikuwa mkamilifu na mwema kabisa (Ezekiel 28:14-15,17), lakini kwa kupenda ubinafsi na kutamani nafasi ya Mungu (Isaya 14:13-14) alianzisha Pambano Kuu.

Katika uasi wake mbinguni Lusifa alitafuta malaika wengine wa kumuunga mkono, na hatimaye

"Kulikuwa na vita mbinguni; Mikaeli na malaika zake wakapigana na yule joka, yule joka naye akapigana nao pamoja na malaika zake; nao hawakushinda, wala mahali pao hapakuonekana tena mbinguni. Yule joka akatupwa, yule mkubwa, nyoka wa zamani, aitwaye Ibilisi na Shetani, audanganyaye ulimwengu wote; akatupwa hata nchi, na malaika zake wakatupwa pamoja naye." Ufunuo 12:7-9.

Malaika huyu muasi, Lusifa, ambaye sasa anajulikana kama shetani, siku zote amekuwa akitoa madai yake kwa viumbe wa Mungu kwamba Mungu hana upendo, kwamba Mungu ni mbinafsi, mwenye kutaka maslahi yake mwenyewe bila kujali maslahi ya viumbe aliowaumba. Hiki ndicho kilikuwa kiini cha vita ile mbinguni, tabia ya Mungu aliwasilishwa vibaya na Lusifa kwa wale malaika wengine na hatimaye "Kuliwa na vita mbinguni" Ufunuo 12:7

Ashukuriwe Mungu kwamba shetani hakushinda vile vita mbinguni, na tena Mungu ametuhakikishia kupitia Neno lake kwamba hata vita vinavyoendelea dunia shetani hatoshinda na tayari alishashindwa pale msalabani. Jipe moyo ndugu mpendwa, shida, maumivu na matatizo yote yakupatayo ni kwamba ni hiki kitambo tu, kwani Mungu wetu atairejesha duniani katika uzuri wake wa awali.

Mpya kutoka kwetu