Pambano Linaendelea

Pambano Linaendelea

"Mungu akaona kila kitu alichokifanya, na tazama, ni chema sana. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya sita" Mwanzo 1:31

Dunia ilipotoka mikononi mwa Mungu kila kitu kilikuwa chema. Lakini leo ni dhahiri kwamba mambo hayapo shwari kwani Dunia yetu sasa ndio uwanja wa mapambano kati ya wema na uovu, pambano hili lililoanzia mbinguni (Ufunuo 12:7-9) sasa lipo duniani.

Biblia inaeleza kwa undani namna ambavyo Dunia yetu iliingia katika pambano hili. Katika Mwanzo 3:1-7 Biblia hueleza kwamba wazazi wetu wa kwanza Adam na Hawa walipoyaamini maneno ya uongo ya nyoka (shetani) walikwenda kinyume na sheria ya Mungu, ndipo tangu hapo dunia yetu ikawa chini ya shetani, utumwani mwake. Maana maandiko yasema...

"Hamjui ya kuwa kwake yeye ambaye mnajitoa nafsi zenu kuwa watumwa wake katika kumtii, mmekuwa watumwa wake yule mnayemtii, kwamba ni utumishi wa dhambi uletao mauti" Warumi 6:16

"Hakuna mtu awezaye kutumikia mabwana wawili" Mathayo 6:24

Katika pambano linaloendelea hapa duniani shetani hutafuta njia za kuwafanya wanadamu wamwasi Mungu kwa kutenda dhambi, kwani anafahamu wazi kabisa kwamba vita tayari alishashindwa hivyo anatafuta wengi awapoteze waweze angamia pamoja naye mwishoni mwa pambano.

Shetani amekuwa akifanya kazi kwa bidii sana katika nyakati hizi za mwisho za Pambano Kuu. Biblia inasema

"mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze." 1 Petro 5:8.

Jambo la kusikitisha ni kwamba wengi leo tumefumbwa macho na shetani hatutambui namna afanyavyo kazi ili kuwapoteza watu, yeye huwapotosha watu wasitambue ukweli kuhusu Mungu na badala yake waamini uongo wake.

Shetani leo hufanya kazi kwa namna tusivyoweza kudhania, hususani kuleta mafundisho potofu ndani ya dini na madhehebu mengi ili kupitia mafundisho hayo mapotofu aweze kumwakilisha Mungu vibaya. Na ndio maana leo ipo idadi kubwa sana ya dini na madhehebu duniani, haukuwa mpango wa Mungu kuwe na machafuko hivi, ni mpango wa shetani katika kuwachanganya watu washindwe kujua ukweli kuhusu Mungu.

Lakini pia shetani leo huwafanya watu wasumbukie mambo ya Dunia tu na wasahau kabisa kutafuta kumfahamu yeye Mwumbaji wao. Wengi leo wamedumbukia katika dimbwi la kutafuta mali na anasa za dunia tu, wengi leo hawapendezwi kabisa na mambo matakatifu ya Mungu. Lakini, si ajabu kwa maana Shetani yupo kazini.

Rafiki shetani anawakokota wengi kuelekea katika upotofu, hebu jitazame na ujihoji mahali unaposimama, pengine ni mambo ya dunia hii ndiyo yaliyokufumba macho ukamsahau Muumba wako?, au pengine umepofushwa na mafundisho potofu ya dini yako yasiyojengwa katika Maandiko Matakatifu, na yenye kumwakilisha Mungu vibaya? Nikukumbushe rafiki shetani anakokota wengi kuelekea katika uangamivu. Hebu wahi leo jiweke katika mikono salama ya Mwokozi wetu Yesu Kristo akuongoze Maisha yako kuelekea katika uzima wa milele.

Mpya kutoka kwetu