Mwisho wa Pambano

Mwisho wa Pambano

Kila wakati unapofungulia redio yako kusikiliza taarifa ya habari, kwa sehemu kubwa hutoacha kusikia taarifa mbaya za kuogofya, za mambo yanayotokea duniani – ajali, vita, njaa, maafa ya asili, mauaji ya kutisha na ukatili wa kila namna. Kweli hali si shwari Duniani!

Biblia inaelezea hali ya dunia yetu sasa katika maneno ya Nabii Isaya, yasemayo

"Dunia inalewa-lewa kama mlevi, nayo inawaya-waya kama machela; na mzigo wa dhambi zake utailemea; nayo itaanguka, wala haitainuka tena."

Isaya 24:20.

Dunia yetu ipo katika hali mbaya kutokana na pambano linaloendelea ndani yake, Pambano Kuu baina ya wema na uovu, pambano ambalo sasa linamhusu kila mkazi wa dunia hii, kuanzia watoto wadogo hadi watu wazima, haijalishi ni mfuasi wa dini au la! Pambano hili linawahusu wanadamu wote, iwe kwa kupenda ama si kwa kupenda wote tunahusika. Na mara zote huwa tunasimama katika upande fulani, wa Jemadari Yesu Kristo ama wa Mkuu wa uasi Shetani.

Ni kweli na dhahiri kwamba ulimwenguni kuna shida nyingi, Bwana wetu Yesu alisema

"Ulimwenguni mnayo dhiki; lakini jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu." Yohana 16:33

Tangu awali adui shetani amekuwa akifanya kazi ili kuwapotosha watu wamtazame Mungu vibaya, wamwone Mungu kama ni mmoja asiye na upendo na asiyejihusisha nao, wamwone Mungu kama Jaji mkali anayewawinda na kuwatafutia makosa ili awaadhibu. Lakini ashukuriwe Mungu kwani kwa kifo cha Yesu pale Msalabani tabia halisi ya shetani ilionekana, kwamba ni mwongo, baba wa uongo na mwuaji kwa asili (Yohana 8:34).

Pia kifo cha Yesu msalabani kilituonesha namna Mungu alivyo, hutuonesha "Mungu ni Upendo", Kifo cha Yesu msalabani kinaonyesha kwamba Mungu anatupenda sana kuliko hata uwepo wake mwenyewe kwa kuwa tayari kufa ili sisi tupone. Kwa maana Yesu alikufa na AKAFUFUKA tulihakikishiwa ushindi wetu dhidi ya mwovu shetani, tunalo tumaini la uzima wa milele kupitia kwa Yesu Kristo Bwana Wetu, japo twaweza kufa hapa Duniani, ni kitambo tu! Tutafufuliwa na Bwana wetu Yesu.

Rafiki habari njema ni kwamba mwisho wa pambano umekaribia, na hadi sasa tayari ushindi upo kwa Yesu Kristo Bwana wetu. Yohana aliandika

"Kisha nikaona mbingu mpya na nchi mpya; kwa maana mbingu za kwanza na nchi ya kwanza zimekwisha kupita, wala hapana bahari tena... Naye [Mungu] atafuta kila chozi katika macho yao, wala mauti haitakuwapo tena; wala maombolezo, wala kilio, wala maumivu hayatakuwapo tena; kwa kuwa mambo ya kwanza yamekwisha kupita."

Na pia tunaambia na Mtumishi wa Mungu Nahum kwamba,

"Mateso hayatainuka mara ya pili" Nahum 1:9

Hivyo basi jipe moyo na mkabidhi maisha yako Yesu akuongoze ili nawe uwe mshindi.

Mpya kutoka kwetu