Kufunika Aibu Yetu

March 3, 2018
March
S M T W T F S
1 2 3
4 5 6 7 8 9 10
11 12 13 14 15 16 17
18 19 20 21 22 23 24
25 26 27 28
S M T W T F S
1 2 3
4 5 6 7 8 9 10
11 12 13 14 15 16 17
18 19 20 21 22 23 24
25 26 27 28 29 30 31
S M T W T F S
1 2 3 4 5 6 7
8 9 10 11 12 13 14
15 16 17 18 19 20 21
22 23 24 25 26 27 28
29 30

Kufunika Aibu Yetu

Dhambi huvunja mahusiano baina ya mwanadamu na Mungu, nayo huleta aibu na hatia rohoni mwa mwanadamu ambayo ni Mungu pekee awezaye kuiondoa. Tazama hali ya kwanza ya wanadamu pale bustanini, Edeni. Biblia inaeleza, walijificha kutoka kwa Mungu (Mwanzo 3:8) pia walipotambua kwamba wapo uchi

"wakashona majani ya mtini, wakajifanyia nguo." Mwanzo 3:7

Awali Adamu na Hawa hawakutambua kwamba wapo uchi kwani walivikwa vazi la utakatifu wa Mungu (Mwanzo 2:25). Lakini baada ya dhambi walifumbuliwa macho wakatambua wapo uchi kwani hawakuwa na utukufu wa Mungu tena, hivyo wakashona mavazi ya majani ya miti kuwa nguo.

Kuna somo muhimu sana katika kisa hiki cha Adamu na Hawa kwa kila mkazi wa Sayari yetu leo. Mara nyingi wanadamu huwa tunajaribu kujifanyizia mavazi yetu wenyewe pale tunapogundua tumepungukiwa na utukufu wa Mungu, hatuna vazi la utakatifu wake na hivyo kama ilivyokuwa kwa Adamu na Hawa, tunajifanyizia mavazi ya majani ili kuficha aibu na hatia yetu.

Hebu tafakari rafiki, ni yapi mavazi uliyojifanyizia leo? pengine ni anasa za dunia hii mwetu, pengine umaarufu, pengine ni uraibu wa vileo...fikiri juu ya chochote kile ukifanyacho ili kufunika aibu na hatia ya dhambi iliyopo miyoni. Lakini ukweli ni kwamba Kamwe hatuwezi kupata mbadala wa vazi la utukufu wa Mungu, hatuwezi kuondoa hatia ya dhambi kwa chochote cha dunia hii.

Biblia inatuambia

"Bwana Mungu akawafanyia Adamu na mkewe mavazi ya ngozi, akawavika." Mwanzo 3:21

Ni Mungu pekee ndiye awezaye kutupatia mavazi ya utakatifu, aliwapatia wazazi wetu mavazi yale ya ngozi. Kupitia mavazi yale aliyowapatia aliwafundisha kitu muhimu sana ambacho hata leo inatupasa kujifunza. Ngozi ile ilitoka kwa mnyama, mnyama (mwana kondoo) ambaye alipasa auawe, achinjwe, ili ngozi yake ichunwe itumike kama vazi, mnyama yule hakuwa na hatia lakini vazi lake liliwafunika wale waliokuwa na hatia.

Mnyama yule aliyechinjwa na ngozi yake kuwapatia wazazi wetu wa kwanza kama vazi anamuwakilisha Yesu Kristo. Yohana Mbatizaji alisema

"Tazama, Mwana-kondoo wa Mungu, aichukuaye dhambi ya ulimwengu!" Yohana 1:29.

Yesu Kristo, Mwana wa Mungu hakuwa na hatia, hakushiriki katika uasi wetu lakini kwa upendo alikubali kutoa maisha yake ili aweze kutufunika kwa vazi la utakatifu wake.

Rafiki, hakuna njia nyingine ya kufunika aibu na hatia ya dhambi zetu, hakuna njia nyingine ya wokovu wetu pasipo kumtazama 'Mwana kondoo wa Mungu azichukuaye dhambi za ulimwengu'. Inatupasa kukubali dhambi zetu, kukubali ukweli kwamba hatuwezi kufunika aibu na hatia za dhambi zetu kwa kujitengenezea wenyewe mavazi ya majani ya miti, ni lazima tunyenyekee miguuni pake yeye aliyetoa uhai wake ili kutuwezesha sisi kuwa hai milele kwa kutuvika vazi la utakatifu wake.