Jifunze Neno

jifunze neno la Mungu

Header Ads

HERI MASKINI?

"Heri walio maskini wa roho kwa maana ufalme wa mbinguni ni wao" Mathayo 5:3

Sauti yenye mguso na kusihi kwa upendo ilisikika kutoka katika mlima ikipenya katika umati wa watu waliokuwa wameketi wakimsikiliza Mwokozi wa Ulimwengu akihubiri mambo ambayo "makutano walishangaa mno kwa mafundisho yake." (Mathayo 7:28). Walishangaa kwa sababu maneno yale yalikuwa mapya masikioni mwao, sio kama walivyozoea kusikia na kufundishwa na viongozi wao wa dini.

Katika jamii ya Wayahudi wa kipindi cha Yesu maneno "Heri walio maskini wa roho" yalikuwa kinyume kabisa na fikra zao. Kwa sehemu kubwa Wayahudi hususani viongozi wa kidini walijiona kuwa wao ni matajiri wa kiroho, kwani wao ndio taifa teule wa Mungu. Jambo hili ni dhahiri hata katika mfano alioutoa Yesu ambapo kulikuwa na Farisayo mmoja aliyeomba moyoni mwake maneno yafuatayo:

"Ee Mungu, nakushukuru kwa kuwa mimi si kama watu wengine, wanyang'anyi, wadhalimu, wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru. Mimi nafunga mara mbili kwa juma; hutoa zaka katika mapato yangu yote. " Luka 18:11

Kauli ya Farisayo huyo iliwakilisha kwa sehemu kubwa hali ya taifa zima, namna ambavyo walikuwa wakijiona kuwa wao ni matajiri wa kiroho, yaani wamekamilika. Lakini ajabu kwa mshangao wanamsikia Yesu akija na maneno yake ambayo yaliwaacha midomo wazi kwa mshangao.

Lakini Yesu alimaanisha nini aliposema 'heri walio maskini wa roho'? Ni swali muhimu kujiuliza. Lakini awali ya yote yatupasa tutambue kwamba maneno hayo yamejaa habari njema mno. kwani kauli hii ya Yesu inaanza na baraka, yaani, 'heri', 'wamebarikiwa', 'wamebarikiwa walio maskini wa roho'. Ni muhimu kufahamu hawa maskini wa roho ni akina nani au wakoje kwani hao ndio warithi wa ufalme wa Mungu.

Neno 'maskini' katika tafsiri rahisi ya lugha humaanisha 'mtu mwenye uhitaji', vivyo hivyo maskini wa roho ni wale ambao roho zao zina uhitaji yaani wanalitambua hitaji lao la kiroho, wanaotambua kwamba ni wadhambi, wapungufu, wakosaji na wasioweza chochote kwa nguvu zao wenyewe na wanatambua hitaji la Mwokozi. Kwao maneno yanatolewa, "Heri walio maskini wa roho kwa maana ufalme wa mbinguni ni wao". Ni kama vile Petro baada ya kuona muujiza mkubwa alioutenda Yesu katika chombo chao cha kuvulia samaki, alijiona dhaifu na mpungufu wake, kisha akasema:

"Ondoka kwangu, kwa kuwa mimi ni mtu mwenye dhambi, Bwana." Luka 5:18

Hapa lipo fundisho kubwa kwetu kujifunza, wanadamu sisi ni wadhambi, mawazo na matendo yetu ni maovu lakini inasikitisha kwamba wengi hatujautambua umaskini wetu wa kiroho, wengi hata miongoni mwa wale wanaodai kuwa wafuasi wa Kristo, viburi, kujikutuza nafsi na kujiona wakamilifu vimejaa mioyoni.

Bwana anatamani sana nawe uweze kuurithi ufalme wa mbinguni, lakini kumbuka ufalme huo ni wa wale walio maskini wa roho. Hebu fanya hili liwe ombi lako daima, muombe Bwana akuonyeshe umaskini wako wa kiroho, muombe akusaidie  upate kuiona hali yako ya kiroho kupitia jicho lake na si macho ya kibinadamu yadanganyayo.
HERI MASKINI? HERI MASKINI? Reviewed by David machibya on 1:51 PM Rating: 5

Ad Home

Programs

GUNDUA

Orodha ya masomo 26 yatakayogusa maisha yako kwa namna ya pekee katika kumjua Mungu, maisha yetu na ukweli wa Biblia

Tazama Orodha >>
NENO LA SIKU

masomo yatakuwezesha kila siku kumkaribia Mungu kupitia tafari za Neno la lake takatifu.

Tazama Orodha >>
AFYA

Pata makala mbalimbali za afya zitakazokuelimisha juu ya kanuni mbalimbali za afya na nini ufanye ili uwe mwenye afya njema.

Tazama Orodha >>
Powered by Blogger.