Jifunze Neno

jifunze neno la Mungu

Header Ads

Wenye Huzuni

"Heri wenye huzuni; Maana hao watafarijika. " Mathayo 5:4

Maisha ya Kikristo ni safari yenye kupiga hatua moja moja kuelekea katika kimo cha ukamilifu wa Mwokozi wetu Yesu Kristo. Mkristo anapaswa kila siku kwa maombi na juhudi, akimtegemea Mungu kutafuta kuyajua mapenzi ya Mungu na kuyatenda.

Katika hubiri la mlimani (Mathayo sura ya 5 hadi ya 7) Bwana wetu Yesu Kristo alifundisha mambo muhimu sana katika safari ya maisha ya Kikristo. Maneno na mafundisho yake pale kwa kweli yaliushangaza umati wake. Si watu wale wa kipindi kile cha Yesu tu, lakini hata kipindi hiki tunachoishi mambo mengi aliyoyasema Yesu hutushangaza fikra zetu leo. Hebu fikiria juu ya maneno haya aliyoyasema  Yesu,  "Heri wenye huzuni".

Heri wenye huzuni? ndivyo alivyosema, kisha akamalizia "Maana hao watafarijika".
Katika hali ya kawaida hakuna mwanadamu anayependa kuwa na huzuni. Sote tunapenda kuwa na nyakati za furaha katika maisha. Lakini Yesu alisema, 'heri', yaani, 'wamebarikiwa', '...wenye huzuni'. Hebu tuangalie Yesu alimaanisha nini katika maneno hayo.

Kabla ya kutamka maneno hayo, yaani "heri wenye huzuni", Yesu alikuwa ametangulia kusema, "heri walio maskini wa roho" yaani heri wale wanaoutambua udhaifu wao, upungufu wao, uovu wao na hitaji lao la Mwokozi, hao ndio aliowasema kuwa maskini wa roho. Hivyo basi maneno "heri wenye huzuni" yalikuwa yakiwalenga wale ambao Yesu aliwataja kuwa maskini wa roho. Maana yake ni hii: pale mtu anapotambua kuwa Yeye ni mdhaifu, ametenda dhambi na hawezi kujiokoa mwenyewe, anapaswa kuhuzunikia dhambi yake, yaani kuijutia dhambi yake kwa lugha nyingine kuichukia dhambi yake. Kwake mtu huyo maneno ya faraja yanatolewa "heri wenye huzuni; Maana hao watafarijika" Mathayo 5:4

Mpendwa, kupitia mguso wa Roho wa Mungu mwanadamu hujitambua kwamba yeye ni mdhambi, hutambua kwamba ni mkosaji mbele za Mungu wake, lakini mara nyingi wengi wetu huishia hapa katika utambuzi wa dhambi zetu tu! hatupigi hatua muhimu inayofuata, yaani, kuhuzunikia dhambi hizo, kujutia kwa nini tumetenda uovu na kuichukia hiyo dhambi.

Rafiki kuhuzunikia dhambi ni swala la muhimu sana kwani pasipo hilo maungamo na toba zetu hazitakuwa ya dhati na hivyo kuwa machukizo tu kwa Bwana, kwani pasipo kuhuzunikia dhambi mtu hatuwezi kuomba msamaha wa dhati, kwani moyo wake haujaona ubaya wa dhambi aliyoitenda hivyo hajanuia kuiacha kabisa.

Yatupasa kuhuzunikia dhambi pale tunapoanguka, kuichukia dhambi utendayo na kuungama dhambi zetu Miguuni pake Yesu, Maneno yake Matakatifu yanasema kwamba,

"Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote" 1 Yohana 1:9

Mpendwa ni ahadi ya Mungu kwamba pale tutakapohuzunika kwa ajili ya dhambi zetu hakika hatatuacha katika huzuni badala yake "atatufariji". Omba kwamba Mungu akuwezeshe kuichukia dhambi leo na kuiacha.
Wenye Huzuni Wenye Huzuni Reviewed by David machibya on 6:49 PM Rating: 5

Ad Home

Programs

GUNDUA

Orodha ya masomo 26 yatakayogusa maisha yako kwa namna ya pekee katika kumjua Mungu, maisha yetu na ukweli wa Biblia

Tazama Orodha >>
NENO LA SIKU

masomo yatakuwezesha kila siku kumkaribia Mungu kupitia tafari za Neno la lake takatifu.

Tazama Orodha >>
AFYA

Pata makala mbalimbali za afya zitakazokuelimisha juu ya kanuni mbalimbali za afya na nini ufanye ili uwe mwenye afya njema.

Tazama Orodha >>
Powered by Blogger.